Ernest Wamba dia Wamba mponyaji kutoka ndani

Jacques Depelchin
Dennis Maryogo

Tunapaswa kumheshimu Profesa Ernest Wamba dia Wamba kwa kuendelea na kazi ya maisha yake.

The sky and landscape as viewed from the window of a helicopter flying over the town of Matadi, Bas-Congo province, DR Congo. Image credit Myriam Asmani for MONUSCO via Flickr CC.

Kwenye masaa ya mapema ya Julai 15, 2020, kwenye hospitali ya chuo kikuu mjini Kinshasa, aliyekuwa kaka yetu, komredi, mwanafalsafa, mwanahistoria, mshauri mawazo, mponyaji na muota ndoto aliaga dunia. Lakini kama nyota angani bado yupo na uwezo wa kutusaidia kwenye kutuongoza katika nyakati hizi za sasa na zile zijazo, ilimradi tunaelewa nini sana sana alikuwa analenga maishani mwake, na jinsi yeye alivyotambua na kuelewa upuuzi wa wale wanaoendesha sehemu kubwa ya mfumo wa utawala unaong’ang’ania ulazimu wa kusimamia na kumiliki kila kitu.

Kutoka popote pale alipo, Profesa Ernest Wamba dia Wamba angefurahishwa mno na kuzinduliwa kwa SENS, tarehe 3 Agosti, 2020, nchini Burkina Faso, kikundi kinacholenga “Kujitolea na kutokujinufaisha kibinafsi.” Kitendo tunachokiona kwa upande wa wanaoitwa viongozi wanaojirumbikia mali ndani ya mataifa mengi ya kiafrika. Kwenye mataifa haya utajiri wa nchi unachotwa na kuwafaidisha zaidi wale waliopo kwenye asilimia 1 ya raia. Je inawezekana kusitisha huu mwenendo? Hilo ni swali kuu lililotawala maisha ya Profesa Wamba dia Wamba.

Katika mbinu zake binafsi za kutatua matatizo ya msingi zaidi, yaliokuwa yanamkabili mtu binafsi au baadhi ya watu, Profesa Ernest Wamba dia Wamba alikuwa na uwezo wa kutumia fikra na vitendo kama kwamba alikuwa sehemu zote, akiona vitu vyote kutokana na pande na maoni tofauti ya wote, huku yeye mwenyewe akibaki imara kwenye tamaduni yake asilia ya Kikongo. Hii inamaanisha kuwa popote pale alipozungumza na mtu yoyote, alifanyikiwa kufanya hivyo kama vile kutoka ndani ya huyo mtu mwenyewe. Alikuwa na uwezo wa hali ya juu wa kumsikiliza mtu kwa umakini mkali.

Mwezi wa Julai 2019, Prof alihitaji kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuomba pasi mpya ya kusafiria, huku akitegemea na kuaga kuwa ingemchukua kwenye mwezi mmoja kufanya hivyo kabla ya kurudi nyumbani Dar es Salaam. Tukiangalia nyuma, hasa kwa wale waliomjua vizuri, kuwa karibu hivyo na pahala alipozaliwa na alipokulia ni hiari kuwa angetamani pia kutembelea chimbuko lake alipotokea, Sundi-Lutete. Hali halisi ya nchi ya DRC inajulikana vizuri hata kwa wale waliopo nje ya nchi hiyo. DRC ni moja ya nchi tajiri zaidi duniani kwa maliasili na rasilimali za kibinadamu. Hata hivyo bado ni nchi yenye viongozi ambao lengo lao la msingi ni kujitajirisha wao wenyewe binafsi huku wakiacha kuwa raia wa kawaida walio wengi zaidi wanaishi kwenye umaskini wa kukithiri, wanabaki kuwa moja ya jamii maskini kuliko zote duniani.

Kwahiyo tunaposema “kutoka ndani” tunamaanisha kujiweka katikati ya maskini wa wamaskini ili kujipatia fursa ya kupambana pamoja nao kuibadilisha historia.

Kitendo hiki cha kumtukuza mtu ambaye umejifunza mengi kutoka kwake kuliko hata vile utakavyoweza kukadiria, sio jambo rahisi na ni changamoto ya kweli. Nilisikia kwa mara ya kwanza kuhusu Ernest Wamba dia Wamba mwaka 1974, kupitia rafiki yetu wote wawili, nilipokuwa nimekamilisha masomo yangu ya Ph.D. na nilikuwa ninaelekea Los Angeles kuanza kazi yangu ya kwanza. Miaka michache baada ya hapo, nilipokuwa Msumbiji, baada ya miaka minne ya kufundisha chuo kikuu cha Dar es Salaam, aliwasiliana nami kupitia tahakiki aliyoniandikia kuhusu makala ya sehemu mbili niliyoiandika pamoja na Henry Bernstein. Alinitumia uhakiki wake wakunikosoa–“Ujuzi wa Kihistoria Unatambulikaje?” –  Nami nikamjibu huku nikikubaliana naye kwa sehemu kubwa.

Kuanzia hapo tuliendelea kuwasiliana hadi pale tulipopata fursa ya kukutana, uso kwa uso, mwaka 1981 au 1982, wakati nilialikwa kusimamia mitihani kwenye idara moja ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kwenye dunia inayotawaliwa na mifumo ya aina au namna za kuwatambulisha watu kimakundi, kuwatenganisha au hata kuwachukulia kama vile kikabila, bado haiwezekani kuamua wapi ni sehemu sahihi na maalumu ya kumweka Profesa Wamba dia Wamba. Wapo wale wanaomchukulia kama mwanafalsafa, wengine wanamuona kama mtaalamu wa nadharia za kisiasa. Wanaofuata msimamo wa kisiasa wa Karl Marx na wale ambao hawaufuati wote wanamuona na kudai ni mwenzao.

Kwa wengine walio wengi, anaonekana kama binadamu mwema, mtu mkarimu aliyekuwa na uwezo kwa kuwa rafiki wa mtu yoyote dunia hii. Sifa hii ni nadra sana hasa kwa wale ambao wametambuliwa kuwa na kipaji na upeo wa kisomi cha hali ya juu zaidi na wenye tuzo nyingi za kuthibitisha hilo au pia wanasayansi maarufu kwa mfano mwingine.

Kwa maoni yake Profesa Wamba dia Wamba, wazo tu kuwa kila mtu ana fikra linamaanisha kuwa mtu yoyote anao uwezo wa kujifunza kutoka kwa yoyote mwingine. Kihalisia, kanuni hii inatuletea maana kuwa mfumo wa kuweka matabaka kwenye ujuzi au kuelimika ni kitu kichukiwacho sana. Ingebidi tutambue kuwa profesa wa chuo kikuu sio lazima ndio atakuwa anajua au anaelewa zaidi. Profesa wa chuo kikuu ni lazima aelewe kuwa yeye anauwezo wa kujifunza jambo kutoka kwa mtu yoyote, haijalishi muktadha wala mazingira. Profesa Wamba dia Wamba alikuwa anapenda kuwakumbusha watu walioshiriki naye kwenye mazungumzo kuwa hata kama historia inaandikwa na wanahistoria, historia siku zote inabadilishwa tu na umma.

Kwa mfano aliouonyesha yeye mwenyewe, alichunguza jinsi gani nadharia ya ubinafsi inaimarishwa panapo mfumo wa matabaka ya ujuzi, na sio tu kwenye mfumo wa elimu, bali pia kupitia tamaduni iliyopewa kipaumbele kupitia mfumo wa kisiasa na kiuchumi.

Kuundwa kwa misamiati, yenye maneno na dhana kama mashindano na ushindani, ni moja ya njia kuu iliyotumika kuamuru tamaduni ya ukandamizaji ya watu weupe. Kama alivyoelekeza Ayi Kwei Armah, Kwame Nkrumah, raisi wa kwanza wa Ghana, kwenye kitabu chake kuhusu maisha yake, alilalamika kuwa alilelewa na alikua kwenye jamii ambayo haikustaarabika. Pale ambapo walioguswa na huu ukandamizaji wa watu weupe na wao wanajikuta wakisambaza na kusimulia hadithi za kihistoria zinazomuumiza msimuliaji aliyeonewa matokeo yake yanaweza kuwa na madhara mengi.

Kwa upande wa dhamira, au fikra tuseme, Profesa Ernest Wamba dia Wamba alibaki muda wote imara kwenye utamaduni wake wa asili, ambao yeye aliuona una hadhi sawa na utamaduni mwingine wowote, chanzo cha ufahamu na ujuzi, busara, na mvuto uliosambazwa kwa michakato ya kijumla na pia ya kibinafsi kupitia mtu mmoja mmoja. Katika kukabiliana na utamaduni wakikoloni, aliyetawaliwa inabidi ajielewe kuwa sawa au hata zaidi.

Ni kitu rahisi kutambua sifa zote hizi za Profesa Ernest Wamba dia Wamba kama mtu mwenye kipaji cha kipekee na mwenye mawazo ambayo yalikuwa yametangulia muda wake kwa maana sio wengi waliokuwa na mawazo kama yake kwa kipindi chake. Lakini ni kitu kigumu kuelewa aliwezaje kutoyumbishwa na vitu visivyo vya msingi na kubaki makini kwenye muono na muelekeo wake. Hata kama alimsifia Lumumba siku zote, aliwahi kutambua pia kuwa hata Lumumba mwenyewe, pamoja na bidii kubwa, hakufanikiwa kutatua ile changamoto kubwa aliyokabiliananayo kama Waziri Mkuu, yaani kugeuza taifa lililokuwa chini ya ukoloni ulioteketeza maisha ya raia wengi na badala yake kuunda taifa lililojali na kutumikia mahitaji ya raia wake wote, hasa hasa wale waliokuwa wamenyonywa zaidi.

Kwenye jitihada yake yakudumu iliyokuwa na lengo la kuigeuza nchi ili iwe inazingatia manufaa ya raia wake, kwa mfano aliyeutoa Simon Kimbangu kwenye miaka ya 1920, Profesa Ernest Wamba dia Wamba alitumia njia hatarishi ambazo wasomi wengi hukwepa. Matokeo yake ni kwamba alijikuta chini ya ardhi ndani ya moja ya jela maarufu za Mobutu. Wakati huo, mapigano ya kumuokoa kutoka kwa hatma mbaya yalihusisha pande mbili: moja ambayo ilipigania kufanya vitu kimya kimya na nyingine ambayo ilisisitiza kufanya kelele nyingi iwezekanavyo. Upande wa mwisho ulishinda. Mwalimu Nyerere (aliyemjua Profesa Ernest Wamba dia Wamba kibinafsi) alimuuliza Rais Mobutu kwanini alikuwa akimuweka mmoja wa maprofesa wake gerezani. Mara tu baada ya hapo, Profesa Ernest Wamba dia Wamba aliachiliwa na akarudi nyumbani kuendelea kufundisha katika Idara ya Historia katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam, nchini Tanzania.

Alipokutana na hali ambayo alikuwa hayuko tayari kukabiliana nayo, kama ilivyokuwa, kwa mfano, kwenye uasi dhidi ya Laurent Désiré Kabila, aliweza kuielekeza upya ile hali halisi kwa njia ambayo ingefanya kazi kwa faida ya wote, sio tu kwa kikundi kinachovutiwa kutumia nguvu za kijeshi kujipatia madaraka. Kwenye mkutano wa Kongo wa Demokrasia, ambapo alichaguliwa, lengo lilibadilishwa kuwafanya wakongo wote waungane na kufanya kazi kwa pamoja katika kujenga taifa ambalo lingefaidisha kila mtu, na sio tu chombo cha wanaoitwa viongozi kujitajirisha. Miongoni mwa matokeo, hizo harakati ziligawanyika vipande viwili halafu vitatu, na hatimae zikizalisha tena hali na mazingira ya uendelezaji wa mtindo wa kupindua nchi kama njia ya kupata madaraka ya serikali.

Kufuatia kuuawa kwa Laurent Desire Kabila mnamo Januari 2001, pande zote zilizohusika katika vita, pamoja na serikali, zilikubaliana kukutana huko Lusaka kujadili jinsi ya kupanga mazungumzo ya kitaifa ya Kongo chini ya uwezeshaji wa Sir Ketumile Masire, rais wa zamani wa Botswana.

Hata kama mazungumzo ya Kongo, ambayo yalifanyika katika jiji la Sun City, Afrika Kusini mnamo 2002, hayakusitisha mara moja na vita zote (kumi na moja) ambazo nchi hiyo ilipitia tangu uhuru, ilionyesha dhahiri kuwa amani inaweza kupatikana huko DRC na pia kati ya DRC na nchi jirani.

Haijalishi ni sehemu gani ya maisha ya Profesa Ernest Wamba dia Wamba mtu anaangalia, mtazamaji yeyote atavutiwa na kutambua tabia au sifa zile zile: kufuata maadili ya ukweli, uaminifu kwa mshikamano na wale ambao ni wanyonge wa dunia, bila kujali mabadiliko ya hali. Hizi ndizo tabia alizokua nazo muda mrefu kabla ya kuvutiwa na wanafalsafa wa Magharibi kama Merleau-Ponty, Jean-Paul Sartre na Alain Badiou kutaja wachache tu.

Kufuatia uasi huo, wanajamii ya Bakongo walimshtaki kwa kuhusika na kuuawa kwa watu wasio na hatia, haswa miongoni mwa, lakini sio tu, watu wa Bakongo. Alipitia mchakato na utaratibu wa kujikosoa na kuomba msamaha. Ushahidi ulioandikwa na wa mdomo utathibitisha mfano mkubwa wa kitendo hiki kilicholenga kuunda hali na mazingira ya upatanisho kati ya watu.

Sababu ya kukumbuka kitendo hiki cha kipekee inafanana na kuhusiana pia na alichokielezea Alain Badiou kama uaminifu au ukweli wa dhati dhidi ya tukio. Tukio lenyewe kwa upande wa Profesa Ernest Wamba dia Wamba linaweza kuhusishwa moja kwa moja na siasa za ukombozi za watu kama Kimpa Vita, aliyeteketezwa kwa moto mnamo Julai 2 1706 na kwa mwingine kama Simon Kimbangu ambae mnamo miaka ya 1920, aliwasihi wakongo wajikomboe kutoka kwenye utawala wa kikoloni, muda mrefu kabla ya kutokea kwa Patrice Emery Lumumba na chama chake cha  Mouvement National Congolais.

Kuyaelewa kwa kina maisha ya Profesa Ernest Wamba dia Wamba sio kazi rahisi ambayo itahitaji juhudi kubwa ya pamoja kutoka kwa wale wengi aliowagusa, aliowavutia, na aliowatia moyo kuungana naye katika harakati za kupelekea kwenye ukombozi na uponyaji kutoka kwa mfumo wa uharibifu kuzidi yote iliowahi kuanzishwa na wanadamu—ubepari.

Yeye hayuko tena nasi kutusaidia kufanya masahihisho ambayo yeye angeyaona kabla yetu; lakini, kwa kujifunza kutokana na masomo aliyotuachia, katika maandishi yake yaliyochapishwa na yale ambayo hayajachapishwa, tunapaswa kuendelea kujifunza, kuyafanyia kazi, na kuyatumia kwa kukumbushana pamoja alichotuachia.

Kutoka kwa mifano mingi aliyotuachia kufuata, kuna mengi mazuri ambayo yanaonekana, kwahiyo ni rahisi zaidi, kwenye hatua hii, kuzingatia machache: muda mrefu baada ya watu wengi wa umri wake kuchagua kustaafu, Profesa Ernest Wamba dia Wamba alikuwa ameelewa mapema kuwa kustaafu kusingewezekana kwake yeye kwa sababu DRCongo ilikuwa bado inaendeshwa kwa mwenendo ule ule kama ilivyokuwa chini ya Mobutu. Siasa za ukombozi zisingewezekana kupitia kudhibiti muundo ambao haukubadilishwa kimsingi tangu nyakati za ukoloni.

Aliliona kama jukumu lake kuendelea kushinikiza mabadiliko kwa manufaa ya watu wengi wa Kongo, haswa kwa wale ambao wasomi na wenye nyadhifa waliendelea kukanyaga.

Utafiti wa Profesa Ernest Wamba dia Wamba kuhusu mchakato mgumu kama njia ya kidemokrasia ya kusuluhisha migogoro haukuhusiana na “uzawa”, lakini badala yake na uelewa wake wa ukweli kwamba mfumo ya demokrasia ulikuwepo barani Afrika, muda mrefu kabla inavyosemekana ulianzishwa nchini Ugiriki ya Kale.

Kwa jinsi hiyo hiyo falsafa ya Afrika ilikuwa kweli falsafa, na sio tu”hadithi hadithi”, sio aina ya tawi la falsafa ya “watu wa zamani”. Katika akili yake, wanafalsafa kama Spinoza, Leibniz Merleau-Ponty, Jean-Paul Sartre, Alain Badiou waligusia aina za fikra na mawazo ambayo yeye alikuwa ameshazisikia tayari tangu wakati anakua na kuelewa utamaduni wa Kongo kama chanzo cha maarifa sawa na tamaduni nyingine yoyote. Katika mawasiliano yake na Alain Badiou, Ernest Wamba dia Wamba alijielewa na kujichukulia kama mtu mwenye hadhi sawa huku na yeye akifanya bidii  ili kufikia malengo yale yale ya ukombozi kamili kwa wanadamu wote.

Mnamo mwaka wa 2012, alijiunga na kundi la wasomi, Shmsw Bak iliyoandaliwa na Ayi Kwei Armah kutafsiri maandishi ya Wamisri wa Kale, na kuyafanya yawafikie wasomaji wa Kiafrika ambao hawakuzungumzi lugha za wakoloni. Profesa Wamba dia Wamba alitoa tafsiri ya mstari baada ya mstari kwa Kikongo kwa kila moja ya maandishi haya manne ambayo yamechapishwa: SaNhat, Smi n Skty pn, SKHKHT EA, Pthh-hhtp: SANHAT, Maandishi rasmi ya Kemet ya Kale, Hadithi ya Mkulima huyu, Juu ya Upendo, Maagizo ya Ptahotep. Maandishi haya yote yanapatikana kutoka kwa PER ANKH mchapishaji wa ushirika wa Kiafrika huko Popenguine, Senegal.

Ikumbukwe kwamba Wamba dia Wamba aliendelea kuishi kwa kutumia yale aliyojifunza kutoka kwa watu kama Kimpa Vita na Nabii Simon Kimbangu. Kwa kadiri alivyokuwa akiamini mwanadamu hakuweza kudai kuwa mwanadamu kama yeye hakuwa mtu wa imani ya kiroho. Imani ya Kiroho sio sawa na dini au itikadi. Kutokana kwa uelewa wake, wanadamu ambao wamezingatia zaidi nia moja ya kujipatia na kujirumbikia bidhaa na mali za kidunia watateketeza, ndani yao, utashi au uwezekano wa uponyaji dhidi ya uharibifu na balaa za mauaji ya kimbari, utumwa wa viwanda, ukoloni, ubaguzi wa rangi na ukoloni mamboleo. Hii ni moja ya sababu zilizomfanya apendezwe na kazi iliyoanzishwa na Ne Muanda Nsemi, kiongozi wa kiroho ambaye alizindua Bundu dia Kongo.

Ikiwa sisi, marafiki zake, dada zake, makaka na wandugu wake, tunamuelewa na kukubali changamoto ambayo ametuachia, basi tutaweza kuishi kulingana na salamu za rambi rambi zilizotugusa mioyo ambazo tumefikisha kwa familia, na, tukijihusisha na kujituma bila kuchelewa kuendeleza malengo aliyojiwekea mwenyewe: kuleta ukombozi wa wanadamu wote kutoka kwa utumwa wa aina ya maisha ambayo huelekea kwenye udanganyifu, vita vya kudumu, udhalilishaji wa utu na hatimae kujiteketeza.

Kwa kuzingatia viwango vya uharibifu na mateso vilivyoathiri ufahamu ya kipamoja ya wanaadamu, kazi iliyopo inaweza kuonekana kuwa ngumu kupita kiasi na pia isiwezekane. Kazi nzito kama hii itakaribishwa kwa njia ya kukumbuka moja ya misemi mingi ambayo Profesa Wamba dia Wamba alitumia.

Katika mfano huu, tutamkumbuka akituambia wakati akikabiliana na kazi ambayo ilionekana haiwezekani kwamba “kwa kile kisichowezekana lazima tukubali kuwajibika.”

Ni kwa njia hiyo tu ambapo mtu anaweza kuwa mkweli kwenye kumuenzi, kuthamini urithi wake, wakati tukiwa wakweli kwetu sisi wenyewe, wakweli kwenye kupatanisha wanadamu na sio kuendelea kuelekea kwenye ushenzi kama Cheikh Anta Diop alivyoonya.

Afrika ina njia na uwezo wa kujijenga upya, na kwenye mchakato huo, kuunda tena mazingira ya kuishi kwa ubinadamu huku ikirejesha ubinadamu huo huo kwenye ufahamu wa mwanadamu.

Further Reading