Janga la mfumo mpya wa ubepari

Tunaanza uchambuzi wetu kuhusu ubepari jijini Nairobi tukiuliza: Je, kuna kitu kama mshahara mzuri siku hizi?

Image credit Ruaraka Social Justice Center.

Mimi ni Gacheke. Mwaka wa 2017 nilikutana na rafiki yangu Antony Adoyo, ambaye kwa sasa ni mratibu wa jamii na wa utafiti unaoshirikisha wanajamii katika kamati ya uendeshaji wa vituo vya haki ya kijamii, inayoshirikisha sauti za wanaharakati wa jamii mabimbali. Wakati huo alikuwa anajitayarisha kutamatisha masomo yake katika chuo kikuu cha Nairobi, ambapo alikuwa mwanawafuzi wa masomo ya uchumi na fedha.

Adoyo alikuwa na ndoto ya kufanya kazi na Benki Kuu ya Kenya. Ndoto ambayo wanafunzi wenzake pia waliienzi. Walitumaini kuwa watapata kazi yenye mapato mazuri. Tulipokuwa tukijadiliana na Adoyo alinisihi nimsaidie kupata kazi kama mwanaharakati wa haki za binadamu kwenye mashirika makubwa. Nilishangaa kuwa msomi wa chuo kikuu nambari moja nchini Kenya angehitaji msaada wangu kupata kazi ya uharakati.

Adoyo alipohitimu mwaka wa elfu mbili na kumi na saba, alinialika pamoja na rafiki wengine kwenye karamu nyumbani kwao. Aliishi katika nyumba za kukodisha yenye vyumba viwili kule Dandora, mojawapo ya mitaa ya walalahoi ilioko karibu na Mathare. Baba yake aliongoza dua ya kumwomba Mwenyezi Mungu amsadie mwanawe kuleta matumaini na kuiondoa familia yake kwenye umaskini na taabu za Dandora. Tulisherehekea mlo wa chapati kwa nyama. Niliona jinsi familia hii iliyojikakamua kumsomesha mwanao ili aweze kuwaokoa kutoka umaskini.

Wanafunzi wengi hawatakua na uwezo wa kutoa familia zao katika umaskini ama kulipa mikopo ambayo wazazi wao walichukua mradi walipe karo ya chuo kikuu. Ni swala la haki ya kijamii kuwa wanafunzi wengi waliohitimu, wana shahada mbalimbali za uguuzi, kama za udaktari, uchumi, uhandisi na bioteknolojia. Shahada hizi zinawapa taswira ya waliopitia kwa miaka kuhitimu. Ukakamavu unaolipizwa na ukosefu wa kazi kwa miaka mitano baadaye na mingine. Wanaishi katika janga la ubepari kila siku.

Mwanafunzi mmoja wa masomo ya ujamaa aliilalamikia kuwa ameacha kuomba kazi akihofia kuwa huenda akapatana mchuuzi akitumia stakabadhi zake kufunga karanga. Alikuwa ametuma maombi yanayozidi mia na alishuku kuwa stakabadhi hizo zinatupwa kisha wachuuzi wanazitumia kufunga bidhaa vyao.


Mimi ni Lena. Nimefanya vibarua vingi wakati wa likizo za chuo kikuu. Nimetumwa kwenye maskani ya walalahai kupeleka maua yenye maelfu ilhali nalipwa shilingi mia tano tu kwa siku. Pesa hizi ziliishia kwenye nauli na mlo. Kama mhudumu wa mkahawa wa matajiri nililipwa shilingi sitini kwa saa, nilifanya kazi siku sita kila wiki nikisimama kwa saa nyingi kuuzia wanunuzi chakula ambacho siwezi kumudu. Kazi yangu ilizalisha mkahawa maelfu mia. Wengi wa wahudumu wenzangu walikuwa wanafunzi waliohitimu wanaofanya kazi kama watumwa na hawawezi ondoka kwa sababu hawana dhamana kuwa watapata kazi nyingine. Wanajua pia kuna wengi kama wao ambao wanatafuta kazi na watakubali hata nusu ya mshahara yao.

Mama Victor ambaye pia ni mwanakamati wa kamati ya uendeshaji wa vituo vya haki ya kijamii na mratibu wa mama za shirika wahasiriwa na walionusurika (wa ukatili wa polisi na mauaji yasiyo ya haki), alikuwa mjakazi kwa miaka sita katika mtaa wa Eastleigh, makao ya wafanya kazi wa asilia ya KiSomali inayopakana na Mathare. Wanawake wengi wajakazi hutoka Mathare, Kiamaiko, Kariobangi, Korogocho, Kiambiu na mitaa mingine ya walalahoi. Wao huenda Eastleigh kila siku wakiwa na njaa ya kupata angalau shilingi mia moja baada ya kufua kwa muda wa saa tatu ama hata kuosha vyombo na kupewa kati shilingi ishirini na hamsini. Kwa wastani, mwanamke mmoja hulipwa shilingi mia mbili.

Kuna ushindani kutoka kwa waKaramajong na Gisu waliohamia kutoka Uganda ambao wanalipwa elfu mbili au tatu kwa mwezi katika kazi ambayo wengi hulipwa elfu tano. Hii inafanya hali ya kusihi kuwa mbaya zaidi. Kutumia shilingi elfu tano ni ngumu, maana kodi ya nyumba ni shilingi elfu tatu na elfu nyingine mbili ni ya kulisha na kuvisha familia. Hali ya Kufanya kazi pia ni mbaya. Wanawake hawa wananyanyswa na kubakwa. Umaskini ni ukatili. Ni mapambano ya ya watu wanaong’ang’ana kuishi katika hali duni.

Tulipo jadiliana na rafiki zetu wengine tulijulishwa kuhusu hali nyingine duni wa wafanyi kazi wa viwandani, sana sana wanawake, wanaofanya kazi kwenye mashamba ya maua, kampuni ambazo zinasafirisha maua na mboga ambavyo vinakandamiza wafanyikazi. Kampuni hizi zina mitambo ya kuchunguza wafanyikazi kwa kutumia alama ya vidole kuhakisha kuwa wameigia saa tatu na dakika ishirini na tisa, asubuhi na kuondoka saa kumi na dakika ishirini na tisa jioni. Kuchelewa hata kwa dakika moja husababisha mkato wa mshahara ambao ni shilingi mia sita sitini na tatu kwa siku. Saa za ziada hazilipiwi. Nchi za ulaya zikihitaji maua nyingi misimu fulani wao hufanya kazi kwa saa ziada kwenye baridi nyingi. Sekta hii ilipata shilingi billioni 153 mwaka wa 2018, ilhali wafanyi kazi hawa wanashinda kwenye baridi bila vifaa wala nguo za kuwakinga. Mfanyikazi mgonjwa hufutwa kazi badala ya kampuni kusimamia matibabu yake. Wakuu wao hufungua akaunti bila idhini ya wafanyikazi, maana wana nambari zao za siri. Sababu ya hii, wanaweza kutoa fedha zao wanavyotaka.

Katiba mpya ya Kenya (2010) na sheria za uhusiano wa kazi 2007 inawapa wafanyikazi haki ya kujiiunga na jumuiya. Kampuni hizi wanawachuguza wafanyikazi, na yeyote anayehusika na jumuiya hufutwa. Majumuia yaliyoko pia yanawakandamiza kwa kuwalipisha ada ila hawajatia bidii katika kuimarisha hali ya wafanyakazi. Wanaendeleza ukatili wa makampuni, serikali na wamiliki nyumba wanaowakandamiza wafanyikazi zaidi kwa kunyonya mapato yao madogo.

Mizizi hii ni ya historia kutoka miaka ya kenda mia na themanini wakati Benki ya Walimwengu na mfuko wa fedha wa kimataifa walilazimisha sera za marekebisho kwenye nchi za KiAfrika, Asia na nyingine kama Kenya. Wakati huo, serikali ya ukoloni ililazimishwa kukatiza uwekezaji katika sekta ya afya, maskani, masomo na kilimo mradi ili wapebari wapate hali nzuri ya kunyonya na kupata faida kutoka kwa huduma hizi ambazo zinafaa kupewa kila mwananchi. Hali hii imekuwa mbaya zaidi msimu huu wa virusi vya korona.

Tunaendelea kupambana na ukandamizaji wa serikali, ukatili na dhuluma za mfumo wa upebari yenye itikadi ya chuki kwa maskini na uchoyo wa faida. Urafiki wetu na Adoyo ulizalisha maandalizi ya masomo ya siasa pamoja na wanafunzi wengine waliohitimu. Kuna shirika la wanafunzi ambalo limeanzisha mafunzo katika mitaa mbalimbali ili watu wapate fahamu ya janga hili la mfumo mpya wa ubepari. Kupitia kwa shirika la wanawake katika vituo vya haki ya kijamii, tunaungana kupambana na unyanyasaji wa wajakazi, ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia. Maktaba ya Ukombozi inaunganisha vituo vya haki ya kijamii na wanafunzi wa vyuo vikuu kwa nia ya kuweka pamoja juhudi zetu na kupambana na ukandamizaji wa serikali, ukatili wa polisi katika vyuo vikuu na ukosefu wa kazi.

Kuunganisha juhudi zetu kati ya wanafunzi na wafanyikazi kunasaidia kutengeneza njia mbadala ya siasa na kutia nguvu muungano wa wanaharakati wa haki ya kijamii kupigania uhuru wa kutoka kwa maisha duni ya ubepari.


Taswira fupi ya hali ya wavujajasho jijini Nairobi:


 

Jackson: Mlinzi /Bawabu

Mkataba: Nilitia sahihi kwenye mkataba kati yangu na kampuni iliyonipa kazi. Inaeleza namna malipo na jinsi kazi inaweza kukatizwa kutoka pande zote mbili. Ina kanuni za kazi. Nafaya kazi siku saba za wiki kutoka saa kumi na moja asubuhi hadi saa kumi na moja jioni wakati huu ambao matembezi yanachunguzwa. Kazi yangu ni kulinda lango na kusahihisha wageni wanaoingia na kutoka.

Hongo: Sikutozwa. Nilisikia kutoka kwa rafiki yangu kwamba kuna kampuni inayotafuta walinzi wa maeneo ya biashara.

Malipo: Nalipwa shilingi elfu kumi na tano kwa mwezi.

Njia ya malipo: Amana kwenye benki

Umbali kutoka kazini: Kutoka Kawangware hadi Kilimani ninakofanya kazi ni kilomita tatu. Natembea nikielekea kazini.

Likizo ya mgonjwa: Kulingana na mkataba, kuna likizo kila mwaka lakini ni vigumu sana siku nzima ya likizo. Lazima nilete noti ya daktari, ila hata hivyo kuna uwezo wa wao kukataa kuniruhusu hata siku moja tu ya likizo. Ni kujikakamua uje kazini ukiwa mgonjwa ama upoteze kazi yako.

Likizo ya uzazi: Hakuna likizo ya uzazi. Wajawazito hawawezi kufanya hii kazi. Ni ngumu. Utajihizulu ama ufutwe.

Fidia: Hakuna. Kuna bima ya matibabu ambayo tunalipia shilingi mia tano kwa kila wakati unapoenda naani hospitali ya kibinafsi. Madaktari pia wanaomba hongo kwa usaidizi wa kupata siku ya likizo.

Athari za kazini: Walevi au wajeuri waweza kusababisha uhamishwe kwenda mbali na nyumbani ama ufutwe kazi. Jumba likivamiwa hatuna namna au vifaa vya kujikinga, pamoja na wale walio ndani.


Mama Victor: Mjakaz

Mkataba: Nafanya kazi ya kufua kutoka jumatatu hadi jumamosi, kutoka saa mbili asubuhi hadi saa kumi na moja jioni.

Hongo: Wakati mwengine unaandikwa kazi kupitia mkandarasi. Kazi inayolipa shilingi elfu tano inabidi umpatie mkandarasi elfu moja kwa kupewa kazi.

Unafanya kazi kwa siku ngapi ya wiki au mwezi: Nilifanya kazi kwa siku tano kwa wiki. Wakati mwingine, siku ya jumamosi kutoka asubuhi hadi mchana kwa shilingi 200.

Malipo Wastani: Shilingi 200 kwa siku.

Njia ya malipo: Pesa taslimu.

Umbali kutoka kazini: Kutoka Mathare 4B(nyumbani) hadi Eastleigh (kazini) ni kama kilomita tatu hivi.

Likizo ya mgonjwa: Hakuna likizo ukiugua. Ukiugua kazini utalazimishwa kumaliza kabla ya kuondoka. Wengine hawajali ikiwa unaugua.

Likizo ya uzazi: Hakuna.

Fidia: Hakuna. Waajiri wengine hukupeleka hospitali na kukuacha huko bila kulipia matibabu.

Athari za kazi: Mashidano kutoka kwa waliohamia nchini Uganda.WaKaramajong na Gisu wanakubali kati ya shilingi elfu mbili na elfu tatu. Ni vigumu kujadiliana ili upate angalau shilingi elfu tano kwa mwezi. Tunapitia unyanyasaji wa kijinsia, na kushambuliwa pia.

Gacheke Gachihi ni mtatibu wa kituo cha haki ya kijamii ya Mathare na mwanakamati wa kamati ya uendeshaji wa vituo vya haki ya haki ya kijamii Nairobi, Kenya.

Lena Anyuolo ni mwanachama wa maktaba ya Ukombozi na Kituo Cha Haki ya Kijamii ya Mathare.Yeye ni mwanaharakati wa haki ya kijamii na mwandishi Nairobi, Kenya.

About the Author

Gacheke Gachihi is the Coordinator of Mathare Social Justice Centre and a member of the Social Justice Centres Working Group Steering Committee in Nairobi, Kenya.

Lena Grace Anyuolo is a writer and social justice activist with Mathare Social Justice Centre and Ukomozi Library.

Further Reading