Ubaguzi wa vijana na mapambano ya kijamii

Vijana masikini wa jiji la Nairobi wanachukuliwa kama wahalifu kwa ajili ya vurugu za mfumo ambazo zinawanyima ajira, haki na uhuru.

Image credit Mathare Social Justice Centre.

Mimi ni Minoo. Nilizaliwa na kulelewa katika kijiji cha Mukuru. Nimeshuhudia aina zote za ukatili wa polisi na ubaguzi wa vijana, pamoja na hali ya umaskini. Nimekutana na vijana kutoka mitaa ya matajiri na ilikuwa wazi kuwa hawajapambana na hali kama hii ya ubaguzi. Hii ni dhibitisho kuwa umaskini ni uhalifu. Mabepari na serikali wanaohalifisha umaskini ndio wanatusukuma kwenye umaskini ili tunapoomba chakula wanavuna jasho letu na kutulipa pesa kidogo zaidi.

Niliamua kuweka rasta kwenye nywele zangu, ila kama mkaazi wa Mukuru Kwa Njenga, nilikuwa na hofu nyingi sana. Niliona jinsi wenzangu walikamatwa wakiwa na nywele zao za rasta, waliaandikiwa mashtaka ya uwongo ya kupatikana na bangi au matendo mengine ya uhalifu. Hali huo mbovu ya vijana umewafanya watu katika jamii pia kuwaona vijana wenye nywele ndefu za rasta kama wahalifu au wanaotumia dawa za kulevya. Nilishuhudia rafiki yangu Kaparo akinyolewa na kipande cha mabati katika kituo cha polisi. Walidai kuwa alikuwa amepigana na mwana wa jasusi wa polisi. Binamu yangu pia na rafiki zake saba walikamatwa kwa madai ya kuwa na bhangi. Yeye na wenzake wane walinyolewa na mapolisi wakitumia wembe moja kati yao. Waliandikiwa mashataka ya uongo kuwa walikuwa wakipanga kuiba. Ilibidii wazazi wao kutoa hongo ili waachiliwe. Mwaka wa 2019, vijana nane wa kiume walipigwa risasi na polisi walipokuwa na mkutano wa kujadiliana kuhusu ukusanyaji wa takataka. Walikuwa na umri kati ya miaka 16 -24.

Nilisomea shule ya msingi ya Mukuru Kwa Njenga iliyokuwa karibu na nyumbani. Shule hiyo ilikuwa na uwanja mkubwa ambao vijana wengi walitumia kucheza mchezo wa kandanda. Lakini, usiku uwanja huo ulikuwa kichinjio. Kijana mmoja aliyekuwa muuzaji wa kitambo wa bangi alipigwa risasi muda wa saa mbili usiku. Polisi walidai kuwa alikuwa mhalifu na kumwekea kadi nyingi za simu na risasi bandia (bonoko).

Kila usiku, hata wakati mwingine mchana, mimi huskia milio ya risasi kutoka kwenye uwanja. Sikupitia ukatili mwingi sana kama mwanamke lakini nimewaona vijana wenzangu wa kiume wakiteseka kila siku. Wakati mwingine, baba yangu husema anamshukuru Mungu kwa kutopata mtoto wa kiume, kisa na maana hajui jinsi angeweza kumlinda dhidi ya ukatili huu unaofanyika katika mitaa ya walalahoi.

Ni hatari kuwa na mavazi za bei ghali kwani inahatarisha maisha yako. Unaweza kushtakiwa kwa wizi na kupigwa kikatili. Najua rafiki zangu ambao hawawezi kuvaa vizuri kwa sababu wamewahi kuwa jela kwa miaka mingi. Hata baada ya kubadili mienendo yao, maafisa wa polisi bado wana mazoea ya kuwanyanyasa, kuwapiga kikatili wakidai kuwa wanataka kujua walikoiba nguo hizo.

Nimenusurika katika huu mtaa nikiona jinsi serikali inavyopata pesa kwa kukandamiza maisha yetu. Serikali inaeneza woga kwa kutumia vurugu na jela. Tunahisi hali ya athari mahali ambapo tunapaita nyumbani. Nina marafiki wasio na hatia wanaozorota gerezani. Kosa lao ni kuwa maskini na kuishi katika mtaa duni. Hatukuchagua hali hii ya maisha.


Mimi ni Maryanne Kasina. Nilizaliwa na kukuzwa Kayole. Nimekua katika jamii iliyojaa udhalimu na najua umaskini ni vurugu. Nilipokuwa shule ya msingi sikuelewa mbona Kayole kulijaa vurugu. Ndoa ya wazazi wangu iliharibika nilipokuwa shule ya upili. Hapo ikawa vigumu sana kutulea. Mamangu alikuwa na watoto kumi. Ilibidi tutoke shuke ya uma na kuenda shule ya kibinafsi iliyo ya bei ya chini ambayo mama angeweza kumudu. Shule ya kibinafsi mtaani ni za bei ya chini, kwa sababu hakuna walimu waliohitimu na mitambo kama maktaba na maabara.
Baada ya kumaliza shule ya upili, hali ilizidi kuharibika nyumbani. Nilifahamu kuwa sitapata karo ya kuendeleza masomo yangu. Tulilala njaa mara nyingi, na kama mtoto wa pili katika familia ya watoto kumi, ilibidi nitafute njia ya kupata chakula.

Rafiki yangu alinieleza kuhusu wakala fulani wa kunisafirisha nje ya nchi kufanya kazi. Nilijua hatari zilizoko. Nilikuwa nimeskia na kuona kwenye vyombo vya habari namna wafanyikazi walivyoona mateso na wakati mwingine hata kifo. Nilihofia sana lakini ilibidi niende. Wakala iliniarifu kuwa wamepata kazi ya uhudumu Dubai tarehe 13 Disemba, mwaka 2013. Mkataba ulikuwa wa miaka miwili. Visa na tikiti ya ndege pia nilipewa. Niliwauliza kama ni kweli nitafanya kazi kwenye hoteli kwa sababu nilihofia zaidi kufanya kazi ya nyumbani kwani wanapitia ukiukaji mwingi wa haki zao. Kilichonishangaza ni kuwa mkataba huu ulikuwa umeandikwa kwa lugha ya kiArabu, na hata hivyo ilibidi ni tie saini. Tarehe 15 Disemba, mwaka huo, nilisafiri kuenda Dubai. Nilipofika na kuelezwa kinachohitajika kwangu kama mfanyi kazi, mwili wangu uliganda na nikatamani kupata mabawa kurudi nchini kwangu. Nilitamani ardhi ipasuke nimezwe lakini wapi. Hali ya kufanya kazi ilkuwa mbovu zaidi.

Niliporudi sikujua kwa kuanzia, kwa maana kila kijana alitumani kuwa ningekuja kuwaoka katika hali zao duni. Walidhani nitawasaidia kupata kazi ngambo bila kujua jinsi hali ilivyo kama jehenamu.Tulikosa njia mbadala na kufadhaika kujimudu, tuliamua kutafuta njia nyingine ya kujimudu kupitia vikundi vya vijana.

Kikundi cha Gaza kilikuwa cha densi tulipokuwa shule ya upili.Tulishindana na mitaa jirani kwa michuano wa kirafiki. Baada ya kumaliza shule ya upili tulitawanyika wengine wakajiunga na vikundi vingine. Vikundi hivi vilifanya miradi ya kukuza jamii na kulinda mazingira. Harakati hizi zilitishia watu fulani, hivyo wakanza kuhusisha majasusi.
Walifanya hivi kwa kuwapea vijana silaha wapiganie ardhi ya matajiri. Vijana walidhani masiha yatabadilika kwani wangepata kipande cha ardhi ya kufanya ukulima na manyumba. Dhana hii iliwafanya kupiga vita hivi na wakashinda, lakini vita hivi vilikuwa vimechochezwa na mfumo. Baadaye, wakaanza kumalizwa, mmoja baada ya mwingine. Ardhi hiyo ilikuja kuuzwa kwa mamilionea wengine.

Nimepoteza rafiki zangu kwa mauaji ya polisi. Wengi niliokuwa nao wamezikwa. Tuliogopa sana kuonekana pamoja kwa hofu ya polisi kutuandama na kutupiga risasi sote, kutukamata ama kutuwekea mashtaka ya uongo ya uhalifu.

Mwaka wa 2017, Rais Uhuru Kenyatta alipeana amri ya kupiga risasi na kuua. Nilishangaa ni nani hawa ambao watauawa? Ni sisi vijana tuliohalifishwa na polisi na ata jamii, pamoja na wanasiasa walio na malengo ya kibinafsi? Sisi ambao tumekuwa mitambo ya kutoa pesa kwa polisi wanotunyang’anya mapato madogo tunayopata? Sisi tulio katika magereza kwa mashtaka ya uongo ya kuwa na bangi na kukosa kutoa hongo?

Idadi ya vituo vya polisi inashinda ya hospitali za uma katika mitaa duni. Serikali inatudhalilisha na kutuua kwa sababu wameshindwa kutupa mahitaji ya kimsingi. Mfumo wa upebari unawanufaisha wachache. Vijana wanapojipanga wanaingiza majasusi katika harakati zao.
Wengine wetu waliokuwa Gaza wanalipa polisi ili waishi. Wengi wetu ni wahasiriwa ama walionusuru haki ya mfumo huu kutojali. Wale ambao hawana uwezo wa kutoa hongo hawana amani. Polisi wauaji wanawaanika mtandaoni na kuwaua.

Nilikutana na Minoo mwaka wa 2018. Nilikuwa namsaidia kuanzisha kituo cha haki ya kijamii ya Mukuru.Tulijadiliana na rafiki wengine wa kike na kuanzisha shirika la wanawake walio kwenye vituo vya haki ya kijamii—Women in Social Justice Centres movement. Shirika hili inachukua hatua za kisiasa. Tunaunda nafasi salama ya watu wote waliokandamizwa. Vita dhidi ya ubepari vinaendelea. Tunafaa kuikumbatia itikadi ya kike kama njia ya kuelekea ujamaa, kurudi kwenye mizizi yetu na utu wetu.

Tunapoangazia maisha yetu na matukio yanaotokea duniani tumegundua kuwa hatuhitaji mageuzi katika idara ya polisi tu, lakini mageuzi ya mfumo wote. Bado tuko chini ya ukoloni. Bado hatujapata uhuru.

Waandishi:

Minoo Kyaa ni mwanachama wa kituo cha haki ya kijamii na Mukuru na kinara wa wanotumia muziki aina ya reggae kueneza haki ya kijamii. Ni mwanachama pia wa shirika la wanawake wa vituo vya haki ya kijamii. Ni mwandishi na mshairi. Sanaa yake inahati mapambano na upinzani.

Maryanne Kasian ni mwandishi na mpatanishi wa wanawake walioko kwenye vituo vya haki ya kijamii nchini Kenya. Yeye ni mojawapo wa waanzilishi wa kituo cha haki ya kijamii ya Kayole. Kituo hiki kinafanya harakati dhidi ya unyasaji wa jinsia ukatili wa polisi.

About the Author

Minoo Kyaa is a member of Mukuru Community Justice Centre and the coordinator of Reggae for Social Justice. She is also a member of the Women in Social Justice Centres movement. She is a writer and a poet. Her art documents struggle and resistance.

Maryanne Kasina is a writer and the convener of Women in Social Justice Centres movement in Kenya. She is the co-founder of Kayole Community Justice Centre which organizes against gender-based violence and police brutality.

Further Reading